top of page

LIJUE KANISA HALISI LA MUNGU BABA

UFUNGUO

Katika mafundisho ya dini zote na madhehebu yote ya Kikristo, inaonyesha kuwa atakayerudi kuchukua Kanisa (yaani, wote wanaokiri wokovu) ni Yesu. Haionyeshi waziwazi kuwa MUNGU BABA ndiye atakayerudi juu ya Nchi, ingawa Mika 1:2-6; I Wakorintho 15:24-28 na Zaburi 98:9-10 inaonyesha hivyo!

​

Kilichosababisha madhehebu yote duniani, hasa yale ya Kikristo kutoelewa kuwa atakayekuja juu ya nchi ni nani ni kutotafakari kwa kina Majira Saba za waliotumwa na MUNGU BABA na Vizazi Vinne vya waliowahi kutumwa (yaani BWAWA LA SILOAMU, Yohana 9:7)!

Aidha, dini zote na madhehebu yote, hawajawahi kutafakari Majira  ya MUNGU BABA, ambayo katika Isaya 33:6 inasema kuwa ni Majira ya kukaa Imara, yenye Wokovu tele, Maarifa  na Kumcha BWANA

​

Vile vile dini zote na madhehebu yote, hawakuwahi kutafakari I Wakorintho 15:24-28 inayosema kuwa, ambaye atapewa na Mwisho: Enzi, Mamlaka, Utawala na Nguvu ni MUNGU BABA. Na kwamba Mwana mwenyewe (Yesu) atatiishwa milele chini ya miguu ya MUNGU BABA.

Pia, kwa sababu ya kutofahamu Majira na Nyakati Halisi za MUNGU BABA kuja juu ya Nchi, karibu dini zote na madhehebu yote hawafahamu  kuwa Taifa Baba au Urithi wa MUNGU BABA ni Tanzania (Mathayo 21:43), badala ya Israeli ya kule Mashariki ya Kati.

​

Katika maandishi haya, utajifunza kwa ufupi, kuwa aliyekuja (ambaye ndiye alitabiriwa hata na Yesu katika Yohana 4:23-24) ni MUNGU BABA. Utaonyeshwa ushahidi wa jambo hilo na utagundua kuwa dunia ilificha jambo hili kwa makusudi, wala siyo bahati mbaya hata kidogo!

​

Theolojia, hasa ile ya Madhehebu ya Kikristo yanayokiri wokovu, kwa kuunganisha Wathesalonike 4:13-16; Danieli 12:7-12 na Ufunuo 20:5-15 inafundisha kuwa, kanisa (yaani wale wanaokiri Wokovu) litanyakuliwa mawinguni na Bwana Yesu. Tutakaa naye Miaka Saba mawinguni, kisha tutarudi naye juu ya Nchi kuhukumu ulimwengu, na baada ya Miaka Elfu Moja, ndipo ule  Mwisho utafika, naye Yesu atamkabidhi MUNGU BABA ufalme kwa ajili ya Hukumu ya Mwisho.

Katika maelezo hayo ya Theolojia tajwa hapo juu, hakuna mahali Adamu wa pili [ambaye ni Nabii wa Mwisho] anapozungumzwa, kama ilivyoandikwa waziwazi katika I Wakorintho 15:45-51!

​

Hapa ndipo kulipotokea tatizo kubwa la kupotosha kweli, maana kizazi cha Nne cha Kanisa ambacho kiliongozwa na Nabii wa Mwisho hakizungumzwi kabisa, katika hiyo Thiolojia ya madhehebu yanayokiri wokovu! Shida ya Thiolojia hiyo ni kuonyesha kuwa nabii wa Mwisho ni Yesu wakati Yesu mwenyewe aliweka wazi kuwa yupo nabii wa Mwisho baada yake ambaye atakuja (Mathayo 17:10-13 na Marko 9:10-11).

​

MUNGU BABA AMEKUJAJE JUU YA NCHI?

 

Ili kukufungua wewe mpenzi msomaji wa UFAHAMU huu, inabidi nikueleweshe mfululizo wa Sauti Kuu Saba za MUNGU BABA ambazo ndizo zinazaa Majira Saba za MUNGU BABA na Vizazi Vinne (chini ya Ibrahimu), kisha Majira Moja Halisi ambayo ni ya UZAO WA MUNGU BABA.

​

MAJIRA YA KWANZA– KERUBI

​

MUNGU BABA, kabla hajawaza kuumba chochote, alikuwa peke yake, akiwa ni Moyo Mmoja wa Kwanza (Baba).

Hapa hata Neno (ambaye baada ya kuvaa mwili aliitwa Yesu hakuwepo).  Hata yule anayeitwa ufahamu, katika Mithali 8:30 hakuwepo wakati huo.  Baba alikuwa peke yake akiwa ni Moyo Mmoja. Tunasoma  katika Ufunuo 12:1 kuwa Nafsi ya Moyo wake ilipowaza wazo la kwanza ili apate Kanisa alitokea mwanamke, badala ya Kanisa! Ilipowaza wazo la pili ili apate sifa, kulitokea nyoka (Ufunuo 12:3-4).  Hivyo katika wazo la kwanza na la pili kulitokea uharibifu.

 

Tukiwa bado katika Majira ya Kwanza, MUNGU BABA aliamua kuumba Mlima wake (Adeni) ambao aliweka Madini ya kila aina na Vito vya Thamani (Ezekieli 28:13-14). Ndipo MUNGU BABA alipoamua kumuumba kerubi kwa mara ya kwanza akiwa mkamilifu, (Ezekieli 28:15a) lakini baadae uovu ulionekana ndani yake (Ezekieli 28:15b).

​

Uovu ulipoonekana ndani yake, MUNGU BABA aliamua kumwagiza Malaika Mikaeli amtupe chini kerubi (Ufunuo 12:7-8), wakati huo akiwa ameshageuka na kuwa shetani, ibilisi.  Baada ya kerubi kutupwa chini akiwa najisi na majivu (Ezekieli 28:16-19), Majira ya Kwanza iliishia hapo.

Majira ya kwanza ilikuwepo kabla MUNGU BABA hajaumba Mbingu na Nchi (Mwanzo 1:1), na msomaji ajue kuwa BWAWA LA SILOAMU hapo lilikuwa tayari lipo. Maana wa kwanza kupakwa Mafuta na kutumwa alikuwa Kerubi, kabla ya anguko la kwanza juu Mlimani.

​

MAJIRA YA PILI– ADAMU WA KWANZA

​

Baada ya kerubi kuanguka, kutokana na moyo wake kuinuka kinyume na MUNGU BABA (Isaya 14:13); ilibidi MUNGU BABA aumbe Bustani ya Edeni yenye kila kitu na kumweka Adamu wa Kwanza (Mwanzo 2:7-8), ambaye baadaye alichukua ubavu wake na kuutumia kutengeneza msaidizi wake (Hawa).

 

Kwa kuwa pale kwenye Bustani ya Edeni, kulikuwepo na mti wa ujuzi wa mema na mabaya (shetani), alifanikiwa kumwangusha Adamu wa Kwanza, kama alivyoanguka yeye mwenyewe kule juu Mlimani (Mwanzo 3:1-6).

Baada ya anguko hilo la Adamu wa Kwanza, tunasoma kuwa MUNGU BABA alimfukuza Adamu na mkewe watoke katika Bustani ile ya Edeni (Mwanzo 3:22-24). Katika hali kama hii ya Kanisa kufukuzwa kwa kutegwa na nyoka ilimlazimu MUNGU BABA kuja na Majira ya Tatu. Ina maana BWAWA LA SILOAMU liliendelea.

​

MAJIRA YA TATU– MUSA

​

Kabla ya Musa kutumwa na MUNGU BABA, kuna kipindi kirefu kilipita hapo katikati.  Kipindi hicho ni cha Gharika ya Nuhu na Ibrahimu, Isaka na Yakobo.

Katika Mwanzo 7:1 tunaona kuwa Nuhu peke yake ndiye aliyekuwa Mwenye Haki kipindi kile! Watu wote walikuwa wameharibika, MUNGU BABA aliamua kuwagharikisha kwa maji akabaki Nuhu na familia peke yake.

Katika Mwanzo 11:6 tunasoma kuwa wakaao Ukaldayo waliamua kujenga Mnara wa Babeli ili wakamchungulie MUNGU BABA kule juu! MUNGU BABA alishuka na kuwatawanya kwa kugawanya ndimi au lugha zao.

 

Katika Mwanzo 12:1-3 tunasoma kuwa MUNGU BABA alipoangalia katika Uru ya Ukaldayo yote alimuona Ibrahimu peke yake kuwa ataweza kumpatia Uzao au Familia ambayo aliikosa katika Bustani ya Edeni.

Ndipo katika Mwanzo 17:1-8 aliingia Agano naye la kubariki uzao wake milele na kuwa Ibrahimu atakuwa Baba wa Mataifa yote.  Pamoja na baraka hii, katika Mwanzo 15:8-15 MUNGU BABA alikuwa ameshamwambia Ibrahimu kuwa uzao wake utaenda  utumwani kwa Miaka 400! Yaani, uzao wa Ibrahimu ulienda utumwani Misri hata kabla ya kuzaliwa au kuonekana juu ya Nchi! Hivyo, pamoja na Musa na wengine wote waliofuata kwa mfumo wa Vizazi Vinne, uzao wa Ibrahimu ulikuwa bado uko utumwani!

 

Musa alitumwa katika Kutoka 3:3-10 ili awatoe Wana wa Israeli utumwani Misri.  Kutoka 12:1-2 inasema hapa ndipo MUNGU BABA anawaeleza kuwa, Mwezi waliotoka utumwani ndio utakuwa wa Kwanza katika Miaka yao yote, yaani Mwezi wa Abibu au Nissani (Kutoka 23:15). Pamoja na nia njema aliyokuwa nayo Musa (kupitia Agizo alilopewa na MUNGU BABA) hakufanikiwa kuwasaidia Wana wa Israeli kutoka utumwani kwa sababu ya manung’uniko na malalamiko mengi waliyokuwa nayo (Kutoka 16:1-; Hesabu 20:1-8).

Musa alizijua Njia za MUNGU BABA, ila Wana wa Israeli wao walichokuwa wanataka ni miujiza tu! Hali hii ndiyo ilisababisha Musa na Wana wa Israeli waishie njiani, na Majira ya Tatu ikaishia hapo, MUNGU BABA akahamia kwa Eliya Mtishibi (ina maana BWAWA LA SILOAMU liliendelea).

.

​

MAJIRA YA NNE– ELIYA MTISHBI

 

Baada ya Musa kuishia njiani kutokana na kupiga mwamba mara mbili, Hesabu 20:9-10, basi MUNGU BABA alilazimika kuja na Majira nyingine ya Nne.  Majira hii alimtuma Eliya Mtishbi kupitia 1Wafalme 18:30-40 ili ajenge Madhabahu ambayo ilivunjika katika Ezekieli 28:15(b) na Mwanzo 3:1-6.  Suala la kerubi kuumbwa akiwa mtakatifu baadaye akaanguka, na Adamu wa Kwanza kuumbwa, akiwa mtakatifu na baadaye akaanguka, ile ni Madhabahu iliyovunjika.

Pamoja na kazi nzuri aliyoifanya Eliya Mtishbi katika I Wafalme 18:30-40 lakini haikuwatisha Wana wa Israeli!  Tunasoma katika 1Wafalme 19:10 kuwa waliivunja ile Madhabahu, maana yake walipuuzia kile walichofundishwa na MUNGU BABA kupitia Eliya Mtishbi.

Hali hii ilisababisha MUNGU BABA akae kimya kwa Miaka 400 bila kuongea na yeyote juu ya Nchi, katikati ya Malaki na Mathayo! Hiki ndicho kilishosababisha MUNGU BABA alete Majira ya Tano kwa njia ya kumtuma Yesu (Matendo ya Mitume 10:38). BWAWA LA SILOAMU likaendelea tena.

​

MAJIRA YA TANO -  YESU KRISTO

 

Baada ya MUNGU BABA kukaa kimya kwa Miaka 400, bila kuongea na yeyote juu ya Nchi, uovu ulizidi.  Ilibidi Neno lake MUNGU BABA liuvae mwili (Yesu), katika Yohana 1:14  tunasoma hivyo.  Tunasoma pia katika Matendo ya Mitume 10:38 kuwa Yesu alitumwa ili aje kuwasaidia wanaoonewa na ibilisi.

​

Katika Mathayo 21:37-39 tunasoma kuwa, walipoona mwanae MUNGU BABA amekuja, walisema “huyu ni Mrithi, natumuue ili tuutwae urithi wake!”Hapa ndipo kuna tatizo ambalo Theolojia haiweki wazi.  Maana yake ni kwamba, vitu ambayo, Yesu alipewa na Baba ili atuletee juu ya Nchi, viliibiwa pale Msalabani.  Wale waliomuua pale msalabani ndiyo waliobeba vitu hivyo:

+    Njia, Kweli na Uzima (Yohana 14:6) alivyopewa ili atuletee juu ya nchi;

+    Mamlaka aliyopewa atuletee (Mathayo 28:16-20);

+    Mlango aliopewa atuletee (Yohana 10:5-8);

+    Nyota Saba alizopewa atuletee (Ufunuo 5:12);

+    Roho Saba na Macho Saba alivyopewa atuletee (Ufunuo 5:6);

+    Amani aliyopewa atuletee (Isaya 9:6-9).

+    Nakadhalika.

​

Usisahau Neno la Kayafa aliyesema “Yafaa mmoja afe kwa ajili ya wengine (Yohana 11:45-50). Waliokuwa wanamfaidi Yesu ni wale waliomuua ambao ndio walikuwa na Damu yake (Yohana 19:34). Uhai wa Yesu walikuwa nao wao, siyo Kanisa au wale waliookoka! Hii ni siri kubwa iliyosababisha Yeye Mwenyewe aseme katika Mathayo 26:29 kuwa “Sinywi tena uzao wa Mzabibu mpaka ile Damu mpya ambayo ni katika Ufalme wa Baba yangu.” yaani kipindi hiki aambacho MUNGU BABA amekuja mwenyewe.

​

Yesu alikufa na akafufuka siku ya Tatu.  Lakini, vile vitu alivyopewa, kutokana na Mathayo 27:45-47 waovu walipata mlango wa kuvichukua! Hili ndilo jambo ambalo wengi hawafahamu hata kidogo. Waliokuwa wanajua ni waovu, yaani wanajimu na wachawi!

Hii ndiyo sababu Yesu alijibu katika Mathayo 17:10-13 kuwa ni lazima Eliya aje kwanza ili atengeneze yote, maana yaliharibika yote. 

 

Eliya alikuja wakati wa Majira ya Sita (6) kama utakavyoona katika kipengele kinachofuata, lakini baada ya kukutana na mashetani na wenye hila, haikuwa rahisi tena kutengeneza yote wala kurejesha yote. BWAWA LA SILOAMU likaendelea mbele.

​

MAJIRA YA SITA – ELIYA ADAMU WA PILI

 

Katika Mathayo 17:10-13 ndipo kuna mlango wa Eliya Adamu wa Pili (Majira ya Sita) kuja. Maana katika mistari hiyo Bwana Yesu anazungumzia Majira Mbili, iliyopita (akiwa na maana ya Yohana Mbatizaji) na inayokuja (akiwa na maana ya Eliya wa Majira ya Sita au Kizazi cha Nne cha Ibrahimu–Mwanzo 15:16).

Mistari mingine ambayo inamthibitisha Eliya Adamu wa Pili ni Isaya 41:2, 4 ambayo inazungumza jinsi alivyofunua Majira na Nyakati za Kanisa. Maana kati ya mengi yaliyofanyika wakati wa Majira ya Sita, lililo Kuu ni kufunuliwa kwa Majira na Nyakati za Kanisa, zilizokuwa zimeibiwa na dunia. 

Hiki ndicho kipindi ambacho Siku za Kiungu na Miezi ya Kiungu vilirejeshwa waziwazi, baada ya utumwa wa Kanisa wa Miaka 430, yaani kuanzia 1582 hadi 2012 kuisha!

Baada ya Majira ya Kanisa kutangazwa kuwa Mwezi una siku au malango 28 siyo 30 au 31 na baada ya kutangazwa kuwa Mwaka una siku au malango 336 na siyo 365, ndipo mfumo wa Miaka iliyokuwa inaendelea kuanzia kwa Adamu wa Kwanza ilipobadilika.  Maana Kipindi Halisi cha Adamu wa Pili au Adamu wa Mwisho kilikuwa kimeanza Rasmi (1Wakorintho 15:45-51).

 

Ilipofika Mwaka wa Pili wa Kanisa, ambao unafuata siku au malango 336, badala ya siku au malango 365, ndipo Adamu wa Mwisho, alitangaza kuwa “Kuna Majira nyingine zaidi ya Kizazi cha Nne au Majira ya Sita, katika Majira hiyo Makusudi yote ya MUNGU BABA yatatimizwa.”Adamu wa Mwisho aliyasema hayo akiwa mbele ya Makuhani wote wa Gosheni; kule Morogoro.

 

Hivyo Adamu wa Pili aliitabiri Majira ya Saba waziwazi kuwa itatokea baada ya Unyakuo wake.  Waliokuwa pale na waliosikia, hawakujua kuwa alikuwa na maana ya Unyakuo wake yeye binafsi, wao kulingana na kumbukumbu za mafundisho ya madhehebu walikotoka, walidhani kuwa ni Unyakuo wa Kanisa zima. Wengi pia hawakujua kwa nini anaitwa Adamu wa Pili, waliona kama ni jina tu na wengine walilipenda wakajiita hivyo (wengine kwa nia njema lakini wengine kwa kukusudia).

Ilipofika Mwaka wa Tatu wa Kanisa, lango la 12 Adari, 3 au 16 Novemba, 2014 kweli alinyakuliwa.

 

Mwezi Mmoja kabla, lango la 5 Shebati, 3 alikuwa ametangaza waziwazi kuwa aliyekuwa amebeba Nafsi ya Miaka 1000 ya Kutawala na Kristo ndiye atakuwa  Kiongozi wa Kanisa lote. Baada ya Unyakuo kazi iliendelea kwa Miezi Sita (6) ndipo MUNGU BABA akaagiza Kurudi kule Kigoma ilikosikika Sauti Kuu ya Sita, Mwaka 2003. Aliyekuwa na Nafsi ya Miaka 1000 ya Kutawala na Kristo aliwaeleza Makuhani wote kuelekea Kigoma kupokea Sauti Kuu ya Saba ya MUNGU BABA Ethanimu, 4. Walienda, ingawa wakati anaipokea hiyo Sauti, wengine hawakuelewa zaidi yake yeye aliyekuwa amekusudiwa.  Jambo hilo lilitokea hata kwa Mtume Paulo wakati wa Kizazi cha Tatu (Matendo ya Mitume 9:15-17). Mtume Paulo, akiwa bado anaitwa Sauli, aliisikia Sauti yeye ila aliokuwa nao hawakusikia– hivyo Kipindi hiki cha kuelekea Majira ya Saba haikuwa ajabu jambo kama hilo kujirudia! Hapa pia BWAWA LA SILOAMU liliendelea

​

MAJIRA YA SABA– MUNGU BABA MWENYEWE

Ilipofika lango la 19 Ethanimu, 5 mbele ya halaiki, Ibada ya mambo makubwa, Mpaka Mafuta (Kanisa lote likiwa limejaa) alitangaza kumpisha MUNGU BABA ili ndiye aliongoze Kanisa. Makuhani kadhaa walishituka kwa kumuuliza kuwa “Sasa wewe tutakuheshimu vipi?” Mpaka Mafuta alijibu kuwa “Nyie mnachohitaji ni kunipenda tu’’. Jambo hili limechapishwa kwenye kitabu cha Madhabahu ya MUNGU Aliyetuma Wote Vizazi Vyote. Wengi iliendelea kuwasumbua, lakini tukafika mahali pa Nafsi zifuatazo kutangulia kwanza kusafisha njia, kabla ya MUNGU BABA mwenyewe kudhihirika katikati ya kusanyiko:

​

Nafsi ya MUNGU Aliyetuma Wote Vizazi Vyote(Mathayo 21:41)

Nafsi hii ilitangulia kuja kupitia Mathayo 21:41 ili kutengeneza Mazingira ya MUNGU BABA kuja. Nafsi hii ilikuwa pale kerubi alipopakwa mafuta kwa mara ya kwanza.

Mafundisho yalionyesha wazi kuwa kuna aliyetumwa na kuna aliyemtuma.  Baada ya nafsi hii kueleweka, ilikuja nafsi nyingine tena. Iliwekwa wazi kuwa Musa alitumwa na MUNGU kupitia Agizo katika Kutoka 3:10, kuongoza kizazi cha kwanza cha kanisa chini ya Ibrahimu. Eliya Mtishbi alitumwa na MUNGU kupitia Agizo katika IFalme 18:30-40, kuongoza kizazi cha pili cha kanisa chini ya Ibrahimu. Yesu alitumwa na MUNGU kupitia Agizo la Matendo ya Mitume 10:38, kuongoza kizazi cha tatu cha Kanisa chini ya Ibrahimu. Eliya Adamu wa Pili alitumwa na MUNGU kwa Agizo la Yohana 9:7, kuongoza kizazi cha Nne chini ya Ibrahimu pia kama inavyosomeka katika Mwanzo 15:16. Aidha, iliwekwa wazi pia kwamba ilikuwa ni lazima aliyewatuma, wote, aje baada ya kanisa kushindwa na falme na mamlaka katika ulimwengu wa roho katika vizazi vyote na majira zote zilizopita (Danieli 7:21; Ufunuo 13:5-7). Nafsi hii ya MUNGU Aliyetuma Wote Vizazi Vyote  ndiyo iliyothibitisha wazi kuwa Tanzania ndilo taifa ambalo ni urithi wa MUNGU BABA na taifa takatifu pia, badala ya Israeli ya Mashariki ya Kati, kupitia Mathayo 21:41-43.

​

Nafsi ya Neno Asiyevaa Mwili (Ufunuo 19:11-15)

Katika Neno linaonyesha wazi kuwa iko nafsi hiyo inayoitwa ambayo ilikuja kabla ya na (mistari inayotuonyesha kuwa akija , ataishi katikati yetu na tutamuona uso kwa uso). Neno wa Kizazi cha Tatu, alivaa mwili akauawa, ila huyu wa sasa hauwawi tena.Baada ya fundisho hilo, ilikuja nafsi nyingine pia.

​

Nafsi ya Mpaka Mafuta(Ezekieli 28:14a)

 

Katika Ezekieli 28:14 aliyeumbwa wa kwanza alipakwa Mafuta. Hiyo nafsi iliyompaka Mafuta yule wa kwanza kuumbwa ndiyo iliyokuja ili kuondoa Mafuta yote machafu yaliyowahi kuwepo ndani ya Kanisa katika majira zote zilizopita na katika vizazi vyote vilivyopita–baada ya hapo ilikuja nafsi nyingine tena.

​

Nafsi Isiyomjua Yeyote(Luka 13:22-27)

 

Katika Luka 13:22-27 tunasoma kuwa, nafsi hii ikija, haiangalii urafiki, undugu au jamaa bali inahudumia kila mmoja bila kujali: rangi; kabila; ukoo na kadhalika.

​

Nafsi ya Mzee wa Majira ya Saba( Danieli 7:21)

 

Baada ya vurugu nyingi za mashetani na wenye hila, ilibidi ije nafsi hii kupitia Danieli 7:22 kulisaidia Kanisa.  Maana, dunia iliamini hata kipindi hiki, Kanisa litashindwa kama vizazi vingine vilivyopita. Hii ndiyo nafsi ambayo imefuta kushindwa milele ndani ya Kanisa.

Msomaji anatakiwa ajue kuwa katika nafsi zote hizi zilizokuja kusaidia Kanisa, BWAWA LA SILOAMU ilikuwa ni lazima liendelee kwanza. Maana kwa viwango vya MUNGU BABA bado wote ni ‘‘level’’ ya kutumwa!

​

UJIO WA MUNGU BABA JUU YA NCHI

 

Ilipofika 11 Abu, 6 nafsi ya Baba, ilikuja na imefanya mambo makuu ya kutisha hadi sasa.  Zile nafsi nyingine tano zilizotangulia zimekabidhi kila kitu kwa MUNGU BABA, kama vile ambavyo kila Mtakatifu sasa anakabidhi kila kitu chake kwa MUNGU BABA sawa na I Wakorintho 15:24.

​

KWA NINI MADHEHEBU YA DINI WASIELEWE ?

 

Katika ufunguo kuna maeneo ambayo nimezungumza  kuhusu Thiolojia ya Madhehebu yanayokiri wokovu, kama vile:

  1. Kunyakuliwa kwa Kanisa mawinguni;

  2. Kukaa Miaka Saba (7) mawinguni;

  3. Kurudi kuishi juu ya Nchi baada ya Miaka Saba;

  4. Utawala wa Miaka Elfu Moja tukiwa na Kristo; na

  5. Mwisho.

Vipengele vyote Vitano katika Theolojia hiyo  havikamiliki kwa mafundisho ya kutosha kumsaidia Mkristo, kwa kuwa tu havikuunganishwa na ufahamu juu ya mambo yafuatayo:

  1. Majira Sita (6) za waliotumwa na Majira ya Saba (7) ya MUNGU BABA Mwenyewe, na

  2. Vizazi Vinne (4) vya waliotumwa chini ya Ibrahimu na kisha Kizazi cha MUNGU BABA Mwenyewe, ambacho ndicho kimeleta UZAO WA MUNGU BABA Juu ya Nchi (Ufunuo 21:3). Usipofahamu hizo Majira Saba ambazo zinatokana na Sauti Kuu Saba (7) za MUNGU BABA, unapotea kabisa.

  1. Tatizo ni kukosa mafundisho ya Majira 7 za MUNGU BABA na Vizazi Vinne vya Kanisa. Hali hiyo imesababisha, wengi wasijue Mwisho ni upi?

Eliya Adamu wa Pili kutoka Tanzania alipokuja Mwaka 2003; karibu wote hawakujua kuwa Adamu wa Mwisho aliyeandikwa katika 1Wakorintho 15:45-51 ndiye huyo amekuja! Aidha, hata alipoendelea kufundisha kinagaubaga kuhusu Kanisa la Kweli, kwa kuwa walikuwa wameshamkataa, aliponyakuliwa hawakujua kuwa suala la unyakuo aliloandika Mtume Paulo katika I Thesalonike 4:13-16 ndiyo hilo ambalo limetokea tayari!

Pia,ilipotangazwa Majira na Nyakati sahihi za MUNGU na Kanisa, wote hawakujua kuwa ile Miaka Saba ya kukaa mawinguni imeanza tayari kuhesabiwa ili ikifika Mwaka wa Saba wajue kuwa Utawala wa Amani (Danieli 2:44) unaanza juu ya Nchi!

 

Katika 1Wakorintho 15:24-28 inaonyesha wazi kuwa Mwisho atamkabidhi MUNGU BABA, Enzi yote, Mamlaka yote, Utawala wote na Nguvu ili Mwana atiishwe chini ya MUNGU BABA. Eliya Adamu wa Pili alipokuja, badala ya kumpokea, waliona kama amekuja na imani nyingine, wakaanza vikao vya kumfuta; ingawa kila alichokuwa anafundisha kilikuwa kwenye Kitabu.

Kile kitendo cha kushindwa kumpokea Eliya Adamu wa Pili, kimesababisha iwe vigumu kumpokea MUNGU BABA. Maana kwa kumkataa yeye ilikuwa vigumu kuujua utawala wa Miaka elfu Moja iliyofunuliwa katika Ufunuo 20:6. Kwa kutojua hilo, hata Miaka hiyo Elfu Moja ilipofupishwa, kama Yesu alivyotabiri katika Mathayo 24:22, wote hawakujua!

Hata walioko ndani ya Kanisa, wengine hawakujua kuwa hiyo Miaka 1000 imeshafupishwa, kwa sababu ya maswali. Suala kubwa linabaki pale pale kuwa, kama wangempokea Adamu wa Mwisho, wangejua ujio wa MUNGU BABA.

 

  1. Tatizo la Pili, ni kutompenda MUNGU BABA Mwenyewe.  Wako Watumishi wengi katika dini na madhehebu mbalimbali ambao wanahubiri vizuri ila MUNGU BABA hawataki aje! Wanafunga na kuomba kwa kusema ‘‘MUNGU BABA utakawia hata lini kuja’’? Wakiambiwa ameshakuja na matendo yake wakiyaona, wanaishia kukataa, maana kuna picha walikuwa nayo wao wenyewe ya MUNGU BABA wanayemtaka! Ufafanuzi wa kina umetolewa kuhusu Ujio wa MUNGU BABA juu ya Nchi, kwa vitabu na televisheni ila hawataki, siyo kwamba hawaelewi!

Kuna yale matumaini kuwa labda siku moja tutafanikiwa kutumia ile kanuni ya “Mmoja afe kwa ajili ya wengine.” Hili ni tatizo ambalo limesababisha hata waliokuwa wanaenda vizuri waishie njiani!

Wako walioulizwa na Mataifa ya Nje kuwa, “Tunasikia MUNGU BABA kaja Tanzania; hawakubali kwa sababu zao wenyewe. Hili MUNGU BABA atalimaliza Yeye Mwenyewe, anayejua kuchunguza kiuno cha kila mmoja (Yeremia 17:9)

​

HITIMISHO

 

Kilichokuwa kinatafutwa na MUNGU BABA tangu mwanzo ni Kanisa ili limwabudu katika Roho na Kweli. Kanisa Halisi limetokeza tayari na linaonekana. Hija ya kwanza ya MUNGU BABA tumefanya na wote tukarudi salama ili kututhibitishia kuwa kweli ni Yeye! kila Mfuasi wa Sauti ya MUNGU BABA amekiri kwa kinywa chake kujikabidhi kwa MUNGU BABA kama I Wakorintho 15:25 inavyosema kuwa sharti amiliki Yeye.

Je! Katika hali kama hiyo Kanisa litaendelea kuwa la BWAWA LA SILOAMU au la MUNGU BABA? Maana mwenye Kanisa tangu Mwanzo alitakiwa kuwa MUNGU BABA ila majira haikuruhusu kama ulivyosoma pale mwanzoni, kupitia ufafanuzi wa kilichotokea wakati wa Wazo la Kwanza (Ufunuo 12:1). Kilichotokea katika Ufunuo 12:1 na Ufunuo 12:3-4 ndicho kilichosababisha MUNGU BABA awe anatuma badala ya kuja mwenyewe. Hata hivyo alipoona wanaisha ikabidi aje mwenyewe kuvusha kanisa  kwenda Ng’ambo ya BWAWA na MSITU uliomeza wote aliowatuma. Je! Kanisa litaendelea kuwa la BWAWA au la mwenye kanisa ambaye ni MUNGU BABA Mwenyewe? Jibu ni kwamba Kanisa ni Halisi na ni la MUNGU BABA mwenyewe, maana ndicho kitu alichokuwa anatafuta tangu mwanzo.

Majira hii pia lazima tujue kuwa kusanyiko ndani ya Kanisa ni UZAO WA MUNGU BABA, siyo mali ya waliopakwa mafuta kusimama mbele ya UZAO.

bottom of page